Loading ...

0
Fursa 101 Africa Academy . 13th Jun, 2021

Biashara ni Mtu Aliye Nyuma Ya biashara

MIMI nyuma ya biashara.

WEWE NI KIZUIZI UNAYEJIZUIA MWENYEWE. MWEKEZAJI HAWEKEZI KWENYE BIASHARA ANAWEKEZA KWA MTU. MWEKEZAJI ASIPOKUAMINI NA KUKUBALI HATA KAMA UNA BIASHARA NZURI YENYE FAIDA HATAKUPA NAFASI.
“M” ya tatu inaitwa MIMI. Narudia tena MIMI …..MIMI…….MIMI mwenye biashara. Biashara ni mtu aliyenyuma ya biashara. Anaweza asionekane lakini uwezo wake ukaonekana.

Kinachoamua mafanikio ya biashara ni Binadamu aliye nyuma ya biashara na siyo mtaji ulio nyuma ya biashara.
Kuna mtu anaweza kuwa na wazo la kawaida lakini akasababisha makubwa kwa mtaji mdogo.
Ninawajua watu masikini wenye mawazo makubwa zaidi ya facebook.
Nimekutana na watu waliokufa kwa stroke wakiwa na zaidi ya Million 100 benki.
Biashara si vitu au mitaji biashara ni mtu aliye nyuma ya biashara.
Ukimchukua Bakhresa na mtu mwingine asiyejua biashara kabisa, wote wakiwa hawana kitu chochote , yaani hata mawasiliano hakuna ukawasafirisha wote nchi ya mbali au parallel universe kama umeona series ya The King Eternal Monarch ya kikorea utaelewa maana ya parallel universe. Haya sasa ukawapa mtaji wa laki tano. Rudi baada ya miaka miwili utakutana na maajabu. Utakutana na Bakhresa yupo juu halafu mwingine yupo mtaani anatafuta kazi au kibarua au ameajiriwa na Bakhresa.
Swali la kujiuliza kwenye biashara ni kwamba unataka nini wewe kwenye hii biashara? Je una mabavu ya kuhimili biashara?
Fahamu kuwa si kila biashara ni saizi yako. Lazima biashara iendane na tabia yako, haiba yako, mapenzi yako, mwonekano wako, vipaji vyako, Imani yako, mategemeo yako, ujuzi wako na msimamo wako. Umeona Fortunata anazalisha Lishe na wewe unataka kufanya , unadhani hiyo biashara inaendana na wewe kweli? Ni saizi yako?

Nakupa mfano hapa wa dada yangu Sabrina Tenganamba alianzisha biashara ya Bar, akamiliki Bar kubwa Morogoro. Anauza bia halafu si mnywaji wa bia. Siku moja usiku nimeenda kumtembelea kwenye bar yake nikakuta anasali ili biashara yake ikue. Nikamuuliza “Yaani unamuomba Mungu akuwezeshe kuuza pombe kwa walevi?”

Akaniambia “Washindani wangu wanatumia wanawake kutangaza bar zao. Kuna Bar inauza sana hapo pembeni kwasababu mmiliki amewaweka wanawake wajiuze ili kuongeza wateja. Mimi siwezi kuwatumia mabinti wa watu wajiuze ili niuze. Ndiyo maana namuomba Mungu aniwezeshe niuze hivyo hivyo bila kutumia wadada wa kujiuza”
Nilicheka sana, nikamwambia. “kama umeamua kuwa moto basi kuwa moto. Kama umeamua kuwa baridi basi kuwa baridi. Mungu na Bar sina uhakika kama vinaendana”

Baada ya muda alifunga Duka na kuanza biashara nyingine. Kumbuka kuwa kuna watu ambao wametajirika kupitia BAR unadhani kwanini? Kuuza Bia ni jambo la kawaida sana, Imani yao, tabia zao na mioyo yao vinafanana na biashara zao. Huwezi kutenganisha hilo.
Nimeona watu wengi wanaingia kwenye biashara zisizo sahihi kwao kwasababu tu wameona wengine wanatengeneza hela kupitia biashara hizo. Na mwisho wa siku wanapoteza kila kitu.
Najua unatafuta kupata hela lakini lazima ujue kuwa si kila biashara ni saizi yako. Lazima uingie kwenye biashara unayofanana nayo.
Kingine lazima uwe na njaa ya kufanikiwa. Usipokuwa na njaa hupati chochote. Biashara ina maumivu mengi Zaidi ya vile unavyofikiri. Kama huna njaa, kama hujadhamiria utaishia njiani. Lazima ujiulize kwanza una malengo gani, una madhumuni gani kwenye maisha yako, unataka nini kwenye maisha yako?

Unasukumwa na nini kwenye maisha yako? Nini madhumuni yako kwenye maisha yako?
Lazima uwe na msukumo mkubwa kama kweli unataka kusafiri safari hii. Safari ya biashara si safari ya wababaishaji. Kuna muda inalazimika kunyakua hadi fursa za watu wengine waliolala. Najua hutanielewa. Mjasiriamali wa kweli hatulii chini kusubiri apewe nafasi….Mjasiriamali wa kweli ananyakua nafasi. Biashara inahitaji Imani nzito kuhusu wewe mwenyewe. Lazima uwe na Imani isiyobabaishwa. Muda mwingine lazima uwe tayari kupoteza chochote kinachokuzuia kwenda mbele hata ikibidi mke au mume. Wafuatilie akina Reginald Mengi nini kiliwakuta kwenye safari ya biashara yakatokea ya kutokea.
Na wala usijidanganye, lazima pia ifike wakati ujue kasoro zako, mapungufu yako na uwezo ulionao.
Kama kuna sehemu inayohitaji uwekezaji kibiashara basi ni hicho kichwa chako. Wekeza kwenye kichwa.
Jambo la kwanza anza kwa kutengeneza maono yako kwenye maeneo makuu ya maisha yako.

Eneo la kwanza ni hela binafsi. Ipende hela. Narudia tena hapa kwa herufi kubwa IPENDE HELA. Kuwa ni binadamu unayetafuta njia za kuingiza hela kwa namna yoyote ile lakini halali. Weka pesa kipaumbele, hakikisha unajua kwa siku unatakiwa kuzalisha kiasi gani cha pesa, kwa wiki, kwa mwezi na kwa mwaka. Kuwa na tamaa ya hela. Yeyote anayekuambia Tajiri hataingia Mbinguni mwambie akuache.
Eneo la pili ni unataka kuwa nani. Unataka utambulikaje, unataka nafasi gani? Jione kama tayari umeshafika kule unakotaka kufika na endesha maisha yako kama tayari umeshafika.
Eneo la tatu ni maisha ya kijamii, hapa unahitaji kuwa na maono ya jinsi unavyogusa maisha ya wengine kwenye jamii.
Eneo la nne ni ujuzi unaohitaji kuwa nao ili upate hela. Ujuzi mkuu unaotakiwa kujifunza ni ujuzi wa kuuza.Chukua kitabu cha Sanaa ya kuuza utanikumbuka. Ujuzi wa kushawishi watu wakupe hela. Jifunze kuongea maneno yanayoshawishi na kuandika maandishi yanayoshawishi.
Eneo la tano jua kile chenye maana kwako. Ni kitu gani chenye maana kwenye maisha yako? Ni kitu gani upo tayari kupambana mpaka kufa kwaajili yake? Lazima uwe na sababu inayosukuma kuishi haya maisha. Kama huna kitu cha maana kinachokusukuma kwenye haya maisha, wewe ni mzigo na huna umuhimu duniani.



Shopping Cart

Loading...