Loading ...

0
Fursa 101 Africa Academy . 13th Jun, 2021

Kuwa na Mental Stamina

Mental stamina “Kuhimili Msongo wa mawazo”
USIPOTEZE MUDA KUJIONEA HURUMA.
“M” ya sita na ya mwisho ni Mawazo na Mtazamo ulionao kwenye biashara. Kuanzisha na kujenga biashara ni stress. Yeyote anayekuambia ni rahisi anakudanganya, biashara ina stress sana hasa kama ni mtu unayeingia kuchezea ligi kuu kibiashara. Wengine wanaweza kukuambia ni rahisi kwasababu ameajiriwa , anapokea mshahara huyo. Sisi wengine ambao maisha yetu yanategemea hilo na tumekutana na mengi mpaka kutafutwa na polisi tunaweza kukusimulia.
Asilimia 90 na Zaidi wanaficha haya, wajasiriamali wengi wakubwa wana maisha yenye msongo wa mawazo sana. Unaweza kuona wanacheka, wamevaa vizuri na wanaongea vizuri na muda mwingine wanasimama kukuhamasisha lakini ukiwafuatilia utashangaa majanga wanayopitia. Nimebahatika kufanya kazi na Eric Shigongo, yule jamaa ukimuona unaweza kudhani yupo sawa.
Mimi nilikuwa naye karibu. Simu yake wanaweza wakapiga simu watu wanaomtukana, unakuta kesi zake mahakamani Zaidi ya tano na anaenda kuzipiga zote.
Mwanzoni nikamuuliza “Bro kwanini kila mara huwa unabadili line ?” alicheka sana. Enzi hizo nilikuwa motivational speaker mkubwa kabla hata hawajatokea wa sasa. Lakini niseme ukweli nilikuwa sijapitia majanga na stress za kunitosha. Ndiyo maana nilipopitia mapito yangu nikaacha kabisa hadi kwenda Redioni ndiyo hicho kipindi akaanza kwenda Joel Nanauka mpaka leo.
Nilipoingia rasmi kwenye ligi kuu ambapo ndipo nilipochukua hela zote nilizokusanya miaka 4 na kuanzisha Chuo, umenunua kompyuta 25, umeweka fenicha na vifaa vyote Chuo kianze halafu umelipia matangazo kwa mtaji wote ukitegemea wanafunzi waje walipe ada ndiyo upate hela ya uendeshaji. Pamoja na matangazo yote bado niliambulia patupu, wanafunzi wachache wengine wanahama.
Hapo walimu wamefundisha miezi minne hawajalipwa mishahara. Wamegoma kufundisha na wanafunzi wameshtaki polisi. Walimu wameshtaki polisi. Bila kusahamu fundi aliyekuwa anasimamia ujenzi amekupeleka kwa balozi. Kila simu unayopokea ni stress. Hapo sijaongelea stress za mahusiano.
Umewahi kuacha gari ukasema utembee kwa mguu upunguze mawazo ukaishia kukaa msituni na kusinzia ? au unatembea halafu hujui unaenda wapi.
Wajasiriamali wengi wanaficha, huwa hawasemi ukweli. Namkumbuka mentor wangu na kaka yangu pamoja ya kwamba anaandika na kuwahamasisha wengine sintamtaja jina, nakumbuka tukiwa ofisini usiku kwasababu tulikuwa tumepanga nyumba nzima yenye uwazi mkubwa na geti. Mimi nikiwa ofisini nikasikia anapiga kelele kwa sauti. Yaani Analia kwa sauti. Nilitoka na mdogo wangu, Director Johor yupo anaweza kusimulia alikuwa Analia kwa sauti. Lakini akitoka nje anaonekana strong na mbabe.
Mjasiriamali asiye na mental stamina, mjasiriamali asiyekuwa na uwezo wa kuhimili mawazo wengi huishia kuwa na msongo wa mawazo. Hata hiki kipindi cha Corona nikisikia mtu aliyeajiriwa anapata mshahara serikalini akisema biashara zifungwe namshangaa sana, hajui madhara makubwa watakayokutana wajasiriamali. Nina list kabisa ya watu ambao wamekufa hivi karibuni baada ya kufunga biashara zao kariakoo. Na si kwamba wamekufa kwa Corona wamekufa kwasababu ya mtikisiko kwenye biashara zao. Nina wajasiriamali kadhaa ambao walikuwa wamesimama vizuri kwenye utalii lakini kwasababu ya Corona wanaumwa. Yaani wanaumwa kweli. Juzi nimekutana na rafiki yangu amekonda sana. Namuuliza “kulikoni bro?” anajibu “wewe acha tu “
Watafiti wanasema kuwa karibu Zaidi ya 50% ya wajasiriamali wanakumbwa mpaka magonjwa ya akili kwasababu ya msongo wa mawazo.
Yaani kwenye biashara kuna presha sana, muda mwingi ni vita ya kwako ukiwa mpweke. Unaweza kuwa na mke au mume lakini asikusaidie kabisa. Yani unateseka mwenyewe. Wengi wanaona mtu ana hela, wanafurahia kunywa bia akiwa amefanikiwa lakini hawajui machozi kiasi gani yalimtoka kwenye safari yake.
Pointi yangu hapa ni kwamba lazima uwe na stamina kimawazo, kiakili na kimtazamo. Usipokuwa na stamina nakuambia ukweli unaweza hata kufa kwenye hii safari ya biashara. Inawezekana usife moja kwa moja lakini msongo wa mawazo hautakuacha salama.
Unatakiwa kufanya yafuatayo ili uwe imara kifikra na uweze kukabiliana na changamoto yoyote kibiashara:
1. USIPOTEZE MUDA KUJIONEA HURUMA.
Usijione mnyonge usiye na uwezo wa kuhimili matatizo. Waache wanyonge walie shida lakini siyo wewe. Wanyonge ni masikini na wabangaizaji lakini siyo wewe. Wewe ni SIMBA usiyeshindwa. SIMBA hajionei huruma huruma kwa lolote. Chochote kinachotokea, anakipokea kama kinavyokuja na kuchagua kuchukua hatua ili maisha yaendelee hata kama ni kufilisika au kifo. Whatever man I don’t care!
Kuna watu wengine wamekuwa wanatumia matukio mabaya yanayotokea kwenye maisha yao kama njia ya kuonewa huruma na wengine, au kutaka kupata msaada kwa wengine. Kwa njia hii wengi wamekuwa wanakaribisha matukio mabaya, au yakiwatokea huwa hawataki yaondoke ili wapate kitu cha kujitetea kwa wengine. Hawa watu ni wanyonge, wewe siyo mnyonge. Umewahi kukutana na watu ambao kila ukiwa nao wana kitu kibaya cha kukuambia kinachoendelea kwenye maisha yao. HAWA WATU NI WANYONGE, WEWE SIYO MNYONGE, UKIWA MJASIRIAMALI USIPOTEZE MUDA KUJIONEA HURUMA KAMA WANYONGE. WEWE NI SIMBA USIYESHINDWA. HII KANUNI ALINIFUNDISHA MAREHEMU REGINALD Mengi
2. USIOGOPE KUCHUKUA HATUA ZA HATARI.
Hakuna mafanikio yanayopatikana kwenye maisha bila ya kuchukua hatua ambazo ni hatari. Kutoka tu nyumbani kwako ni hatari, unaweza kugongwa na gari, unaweza kushambuliwa na watu na kadhalika.
Lakini watu wengi wamekuwa wanaogopa kuchukua hatua ambazo zinaonekana ni za hatari ili kupata wanachotaka kwenye maisha yao, lazima mtu ujue nini unataka, kisha ujue hatari unayohitaji kuingia ili kupata unachotaka, baada ya hapo kuchukua hatua sahihi ili kupata unachotaka, huku ukiwa na mbadala unaozuia hatari yoyote unayokutana nayo isikupoteze kabisa.
3. USIOGOPE MABADILIKO.
Mabadiliko ni kitu ambacho hakikwepeki kwenye BIASHARA, maisha, kama wewe utagoma kubadilika, basi mazingira yanayokuzunguka yatabadilika. Na pale unapostuka na kugundua mazingira yamebadilika, basi jua umeshaachwa nyuma.
Watu wengi wamekuwa wanaogopa kufanya mabadiliko kwenye maisha yao kwa sababu mabadiliko ni magumu. kwa nini watu wengi hung’ang’ana kwenye ajira ambazo zinawalipa kidogo kwa miaka mingi na wasithubutu kuondoka na kuingia kwenye biashara ambazo zinaweza kuwalipa zaidi? Wengi wanapenda kipato kidogo cha uhakika, kuliko kipato kikubwa kisicho cha uhakika.
Ili kuondokana na hali ya kuogopa mabadiliko,hakikisha unajua mabadiliko gani unataka kufanya kwenye maisha yako, kisha chukua hatua ndogo ndogo. Unapochukua hatua ndogo ndogo, unaipunguza hofu ya mabadiliko uliyonayo.
4. USITAKE KUMRIDHISHA KILA MTU.
Watu wengi hufikiri kwamba ili wafanikiwe kwenye maisha basi lazima wapendwe na kila mtu, hivyo hujaribu kufanya mambo ambayo yanawafurahisha wengine, hata kama siyo mambo wanayojali kufanya. Hakuna chochote utakachofanya kwenye maisha na ukamfurahisha kila mtu au kupendwa na kila mtu. Na pale unapoigiza maisha fulani ili kuwafurahisha watu fulani, unavutia watu ambao siyo halisi kwako. Ishi maisha ya uhalisia kwako, hapo utawavutia watu sahihi ambao utaweza kwenda nao vizuri.
5. USIZAME KWENYE YALIYOPITA.
Kuna mambo makubwa, mabaya na magumu sana umewahi kukutana kwenye biashara yako. Kuna watu walikunyanyasa, kukutesa, kukudhulumu na kukuumiza sana kwenye maisha yako. Lakini sasa upo hapo ulipo sasa, unachagua nini? Kuendelea kuzama kwenye yaliyopita au kuangalia wapi unakokwenda?
Namalizia kwa kusema hivi, unapoingia kufanya biashara fahamu kuwa unaingia kwenye maumivu lakini lazima uyakubali na kuona sehemu ya maisha yako
Katika ya ujuzi unaotakiwa kujifunza unapoingia kujenga biashara ni ujuzi wa kukabiliana na changamoto, stress na matatizo yoyote yatakayojitokeza mbeleni.


Shopping Cart

Loading...